1301812

Breaking News: Yanga Bingwa Ligi Kuu

HATIMAYE yametimia Yanga ndiyo mabingwa wapya wa Ligi ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/15, baada ya jioni ya leo kuifunga Polisi Moro mabao 4-1 na kufikisha pointi 55 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote inayoshiriki ligi hiyo kwa msimu huu wakiwemo waliokuwa mabingwa watetezi Azam FC.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuwa mshindi wa kihistoria katika Ligi hiyo kwa kunyakuwa ubingwa huo mara 25 huku wapinzani wao Simba wakishika nafasi ya pili kwa kunyakua ubingwa huo mara 18.

Matokeo hayo pia yameifanya Yanga iliyobakiwa na mechi mbili mkononi kuacha ushindani mkali kwa timu mbili za Azam na Simba zinazo pigania kumaliza msimu huu nafasi ya pili huku timu za Polisi Moro, Ndanda FC, na Tanzania prisons nao wakipambana kutokushuka daraja.

Huo ulikuwa ni mchezo wa nane mfululizo wa mechi za Ligi ya Vodacom Tanzania bara kwa Yanga kucheza bila kufungwa na mechi tatu mfululizo baada ya kucheza na Etoile du Sahel na kushinda zote huku safu yake ya ushambiliaji ikionekana kuwa kali zaidi kwa kufunga mabao 12 huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikishwa mara tatu.

Mshambuliaji hatari Amissi Tambwe alipiga hat- trick yake ya pili msimu huu akiwa na kikosi cha Yanga na kufikisha idadi ya mabao 14 nyuma wa kinara Simon Msuva pia wa Yanga mwenye mabao 17.

Wachezaji wa Polisi Moro waliuanza mchezo huo kwa kasi na kuzua hofu kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa wamefurika uwanjani hapo kushuhudia timu yao ikitwaa ubingwa huo na marakadhaa mshambuliaji wao wa zamani Said Bahanuzi alishindwa kuzitumia vyema nafasi alizozipa na kupiga nje au kipa wa Yanga Deogratius Munish kudaka.

Raia wa Burundi Amissi Tambwe aliwainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao zuri akiunganisha krosi ya Simon Msuva, dakika ya 41 na kurudisha matumaini ya viongozi na benchi la ufundi kufuatia ugumu uliokuwa umejitokeza kwenye dakika za awali.

Polisi Moro walikianza kipindi cha pili kwa kasi baada ya kumtoa Bahanuzi na kumuingiza Nichalaus Kabipe dakika ya 49, lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia timu hiyo na kujikuta wakifungwa bao la pili dakika ya 53 kupitia kwa Tambwe tena akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Polisi Abdul Ibad.

Mpira wa bao hilo ulianzia kwa Msuva aliyepiga shuti kali lilotemwa na kipa huyo na mpira kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.

Tambwe alijihakikishia kuondoka na mpira katika mchezo huo baada ya kufunga bao la tatu (hat-trick) katika dakika ya 59 akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa.

Dakika ya 66,kinara wa mabao kwenye ligi ya Vodacom,Simon Msuva aliifungia Yanga bao la nne akimalizia kazi nzuri ya Ngassa aliyeupenyeza mpira katikati ya mabeki wa Polisi na kufumua shuti kali ambalo lilimshika kipa Abdul Ibad.

Baada ya kufungwa bao hilo Polisi walionekana kuzinduka hasa baada ya kuumia kwa beki Kelvin Yondan na Yanga kuingiza mchezaji mwingine kutokana na kumaliza idadi ya wachezaji watatu na dakiak ya 83 Bantu Admin aliifungia timu hiyo bao la kufutia machozi akipiga shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kujaa wavuni.

Baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Zacharia Jacob wachezaji wa Yanga walivalia T-Shert maalum zilizo andikwa Yanga bingwa 2014/2015 na kuanza kuzunguka uwanjani wakiwa wa kocha wao Hans van der Pluijm wakiwapungia mikono mashabiki wao.

Baada ya mchezo huo Yanga inaingia kambini kesho jioni kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho hatua ya 16 dhidi ya Etoile du Sahel, ambao utapigwa Sousse Tunisia Mei 1.

Yanga:
Deogratius Munis, Juma Abdul,Oscar Joshua, Mbuyu Twitte, Kelvin Yondan, Said Juma, Simon Msuva/ Jeryson Tegete, Niyonzima/Nizar Khalfan, Amiss Tambwe/ Hussein Javu, Mrisho Ngassa na Kipah Sherman.

Polisi Moro:
Abdul Ibad, Ally Teru,Hassan Mganga, Meshack Abel/Bakar Nahodha, Laban Kambole, Anafi selemani, Admini Bantu, Said Mkangu, Said Bahanuzi na Seleman Kassim na James Abrose/Mussa Mohamed.

Advertisement

ENJOYED THIS STORY?

Add GOAL.com as a preferred source on Google to see more of our reporting