Klabu ya Yanga imesema kuwa umepanga kuongeza idadi chache ya wachezaji kwenye kipindi hiki cha usajili ili wasiweze kuvuruga utendaji kazi wa timu ambao hivi sasa umeanza kuchanganya baada ya kucheza mechi tisa za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa, ameiambia Goal, idadi kamili ya wachezaji wanaotaka kuwasajili ni watatu pekee ambao wanacheza kwenye nafasi za kiungo na ushambuliaji.
"Tunataka kuimarisha eneo letu la kiungo pamoja na ushambuliaji unajua tuna washambuliaji wetu wawili tegemeo ni majeruhi hawajaichezea timu kwa muda mrefu, lakini pia eneo la kiungo tunatafuta mtu wa kumsaidia Papy Kabamba na Rafael Daud, ambao bado ni mdogo, na mipango inakwenda vizuri kwa ajili ya kuwapata mbadala wa wachezaji hao," amesema Mkwasa.
Kiongozi huyo amesema mpaka sasa tayari wamefanya mazungumzo na mshambuliaji mmoja kutoka nchini Kongo na kiungo mmoja ambaye ni mzawa wa Tanzania na kila kitu kinakwenda sawa wanachosubiri ni dirisha kufunguliwa ili waweze kukamilisha taratibu na kuwatangaza kuwa mali yao.
Amesema kuhusu mshambuliaji mmoja bado wanamsikiliza kocha wao George Lwandamina, ili kujua ni mchezaji gani ambaye amevutiwa naye na hilo linaweza kukamilika mara baada ya kurudi nchini akitokea kwao Zambia alikokwenda kwa ajili ya matatizo ya kifamilia.
Yanga imekuwa ikipata ushindi wake kwa tabu msimu huu, kutokana na kuwakosa Donald Ngoma na Amissi Tambwe, ambao hawajaitumikia timu hiyo kwa asilimia 100, kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita.
