1205082

Match Report: Yanga 8- 0 Coastal Union, Tambwe atupia manne

TIMU ya YANGA leo imeweweka rekodi mpya kwenye Ligi ya Vodacom Tanzania bara baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga mabao 8-0 katika pambano lililopigwa uwanja wa taifa Dar es Salaam.

Rekodi ya kukumbukwa kwenye mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja ni idadi ya mabao nane sawa na tarehe ya leo na idadi ya mabao manne aliyofunga mshambuliaji wake Amissi Tambwe yameendeana na mwezi Aprili ambao kwa sasa ndio tupo.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 43 na kijiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu huku pia ikiwa inafanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirkisho Afrika CAF.

Mrundi Amissi Tambwe ndiye aliyekuwa shujaa wa Yanga katika mchezo huo baada ya kufunga mabao manne na kufikisha idadi ya mabao tisa kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania bara.

Tambwe alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tisa akimalizia kwa kichwa mpira wa Sherman aliyeurudisha ndani kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa kutoka Kaskazini mwa uwanja wa taifa Dar es Saalam.

Simon Msuva aliifungia Yanga bao la pili katika dakika ya 23 baada ya kuunganisha pasi ya Haruna Niyonzima. Tambwe aliifungia Yanga bao la tatu katika dakika ya 34 akiunganisha mpira wa shuti uliopigwa na Juma Abdul.

Kabla ya bao hilo, Tambwe alikosa bao katika dakika ya 31 baada ya kupiga tick taka na mpira kugonga mwmaba wa juu na kurudi uwanjani.

Mchezaji huyo wa zamani wa Simba alikuwa nyota wa mchezo jana baada ya kufunga bao la nne katika dakika ya 48. na dakika mbili baadae Sherman alifunga bao la tano na lakwanza tangu ajiunge na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili mwezi desemba mwaka 2014.

Yanga iliendelea kuutawala mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi Simon Mbelwa na dakika ya 86 Msuva alifunga bao la sita akitumia vizuri pasi ya Tambwe, wakati mashabiki wakiwa bado wamesimama kushangilia bao hilo kiungo Salum Telela, alifunga bao la saba kwa mpira alioupiga kiufundi akiwa nje ya eneo la hatari na kumshinda kipa wa Coastal Union Bakari Fikirini dakika ya 88.

Wakati mashabiki wakiamini matokeo yatabaki hivyo Tambwe, alihitimisha karamu ya mabao kwa upande wa Yanga dakika ya 90 baada ya kufunga bao la nane akipokea pasi nzuri kutoka kwa Niyonzima na kabla ya kufunga alimlamba chenga kipa wa Coastal Fikirini, na kuujaza mpira wavuni.

Coastal Unioni inayofundishwa na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ilishindwa kabisa kuonyesha ushindani katika mchezo huo licha japo katika dakika za awali mshambuliaji wake Mnigeria Iker Bright na kiungo Abdulhalim Humud kuonyesha juhudi za kukabiliana na wachezaji wa Yanga.

Baada ya kuona mambo magumu kipindi cha pili Julio, aliwatoa Mohamed Ally, Bright na Rajabu Mohamed na nafasi zao kuchukuliwa na Abbasi Athuman, Mohamed Mtindi na Shekuwe Mohamed lakini mabadiliko hayo hayakuweza kumsaidia

Kwaupande wa kocha wa Yanga Hans van der Pluijm, alimwapumzisha Mbuyu Twite, Sherman na Oscar Joshua na nafasi zao kuchukuliwa na Hassan Dilunga, Nizar Khalfan na Andrew Charles na mabadiliko hayo yaliweza kumsaidia kuongeza idadi ya mabao.

Advertisement

ENJOYED THIS STORY?

Add GOAL.com as a preferred source on Google to see more of our reporting

0