Ruvu Shooting imetoa mchezaji bora Ligi Kuu

Abdulrahman amewashinda wachezaji Jafar Salum wa Mtibwa Sugar FC na Zahoro Pazi wa Mbeya City

Mshambulizi chipukizi wa Ruvu Shooting ya Pwani, Abdulrahman Mussa ameibuka kuwa mchezaji bora wa ligi ya Vodacom Tanzania kwa mwezi Aprili.

Msemaji wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Alfred Lucas ameiambia Goal, Abdulrahman amewashinda wachezaji Jafar Salum wa Mtibwa Sugar  na Zahoro Pazi wa Mbeya City.

“Jopo la makocha wememteua Abdulrahman kutokana na mchango wake kwa timu yake Ruvu katika mechi tatu alizoichezea mwezi huu wa Aprili aliweza kucheza kwa asilimia 100 mechi zote tatu na kufunga mabao manne,” amesema Lucas.

Msemaji huyo  amesema kitu kingine kilichochangia mchezaji huyo kuteuliwa ni kasi yake ya ufungaji kwenye ligi ya Vodacom ambapo sasa ana mabao 12 sawa na Simon Msuva wa Yanga mwenye idadi kama hiyo ya mabao.

Abdulrahman alifunga Hat-Trick katika mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Majimaji uliochezwa katika Uwanja wa Mabatini Mlandizi, Pwani.

Kwa kushinda tuzo hiyo, Abdulrahman Mussa atazawadiwa kitita cha shilingi Milioni moja kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, Vodacom Tanzania.

Kwa upande wake mshambuliaji huyo amefurahi kutwaa tuzo hiyo na kusema itamuongezea ari ya kujituma na kuipa mafanikio zaidi timu yake katika mechi zilizobaki kabla ya msimu kumalizika Mei 21 mwaka huu.