GOAL 50

Waandishi Goal kutoka nchi 37 tofauti walipiga kura katika toleo la kumi la tuzo za wachezaji bora 50 wa dunia

50. Thomas Lemar

Baada ya kuanza vema msimu wa kwanza Monaco, alipotua akitokea Caen majira ya joto 2015, Thomas Lemar amekuwa miongoni mwa mawinga wa kusisimua duniani katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alifunga mara tisa klabu yake ilipotwaa taji la Ligue 1, kiwango chake safi kikiishawishi Arsenal kutoa dau la euro milioni 100 kuipata huduma yake siku ya kufungwa dirisha la usajili. Monaco kuikataa ofa hiyo inadhihirisha ni jinsi gani wanamthamini mchezaji huyo mpya aliyeingia Goal 50.

49. Bas Dost

Mmoja wa sajili bora za msimu uliopita, Bas Dost alifunga magoli 34 katika mechi 31 tu akiwa na Sporting CP na kumaliza kama kinara wa mabao katika Primeira Liga, baada ya kujiunga na klabu hiyo akitokea Wolfsburg kwa auro milioni 11 tu majira ya joto 2016.

Kulingana na hayo, Mholanzi huyo, ambaye sasa anahusishwa na tetesi za kutaka kujiunga na Everton Januari, amepata wa fursa ya kuingia kwa mara ya kwanza kwenye Goal 50.

48. Naby Keita

Miongoni mwa nyota wanaoibuka kwa kasi kwenye ulimwengu wa soka, mchezaji mpya katika orodha ya Goal 50 Naby Keita amekuwa kiini cha RB Leipzig kumaliza nafasi ya pili kwenye Bundesliga ya Ujerumani, akifunga mara nane na kutoa pasi saba za goli.

Liverpool walikwa wakitamani sana kumtia mikononi mwao mchezaji huyo wa kimataifa wa Guinea mwenye umri wa miaka 22 ambaye walishakubali kutoa paundi milioni 70 kumnunua mwakani!

47. Diego Costa

Diego Costa baada ya kutokuwa kwenye mipango ya meneja Antonio Conte, imemlazimu kurudi Atletico Madrid, lakini mshambuliaji huyo matata alikuwa na mchango mkubwa katika ubingwa wa Chelsea Ligi Kuu Uingereza 2016-17 na hilo halina ubishi.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania aliiongoza safu ya mashambulizi kwa namna ya kipekee, akifunga mara 20 katika ligi, na anastahili kabisa kuwa kwenye orodha ya Goal 50 kwa mara ya tatu.

46. David de Gea

Hakuna ubishi kwamba ni kipa bora na thabiti kwa miaka mitano iliyopita, David de Gea wakati mwingine hapewi sifa anayostahili, umahiri wake hautiliwi mkazo katika hatua hii.

Hata hivyo, nambari moja huyu wa Manchester United anaingia kwenye orodha ya Goal 50 kwa mara ya tatu mfululizo, alicheza mechi 14 bila kuruhusu goli msimu uliopita Ligi Kuu Uingereza na ameruhusu magoli 29 tu katika mechi 35.

45. Mario Mandzukic

Ikumbukuwe kwamba Juventus walianza kwa kusua-sua nusu ya kwanza ya msimu wa 2016-17. Ilikuwa ni baada ya kutumia mfumo wa 4-2-3-1 Januari – ambao ulimlazimu Mario Mandzukic kucheza winga ya kushoto – Mabingwa hao wa Italia walianza kupaa.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Croatia alijidhihirisha kuwa ni mchezaji muhimu kwenye timu, kwa upande wa mashambulizi na safu ya ulinzi pia, na alifanikiwa kufunga katika mechi zote za nusu fainali Ligi ya Mabingwa.

44. Cesar Azpilicueta

Iwe amechezeshwa kama beki wa kulia au wa kati, Cesar Azpilicueta amekuwa mchezaji wa Chelsea anayecheza katika kiwango cha juu, na alikuwa mtu muhimu katika mafanikio ya Ligi Kuu Uingereza msimu uliopita.

Nyota huyo, mwenye miaka 28 ameonyesha umahiri wake katika mashambulizi pia msimu huu, baada ya kuonesha maelewano mazunri na Muhispania mwenzake Alvaro Morata na amepata fursa ya kuingia kwa mara ya kwanza kwenye Goal 50.

43. Philippe Coutinho

Philippe Coutinho amekuwa mahiri tangu alipojiunga na Liverpool akitokea Inter 2013 lakini amepanda anga nyingine miezi 12 iliyopita, kama ilivyoonekana Barcelona walifanya majaribio kadhaa kumsajili lakini walishindwa majira ya joto.
Kiungo huyo mshambuliaji ameisaidia Liverpool kurejea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa akifunga mabao 13 msimu uliopita, na kuwa Mbrazili mwenye kasi kubwa ya kufunga katika historia ya Ligi Kuu Uingereza.

42. Benjamin Mendy

Maendeleo ya haraka ya Benjamin Mendy hadi kuwa mmoja wa mabeki bora wa kushoto duniani yamethibitika baada ya mwaka mmoja tu kujiunga na Monaco akitokea Marseille kwa €13m, Manchester City wamelipa €57.5m kumhamishia Etihad.

Mfaransa huyo amekuwa na bahati mbaya kwani mapema kabisa mwanzo wa msimu amepata majeraha ya kano ya goti la kushoto Septemba lakini hadi hapo alikuwa ameshafanya makubwa kuonyesha kuwa anastahili kuingia kwenye orodha ya Goal 50 kwa mara ya kwanza, ametoa pasi 11 za magoli katika michuano yote msimu uliopita akiwa na mabingwa wa Ligue 1 Monaco.

41. Fabinho

Alikuwa beki bora chipukizi wa kulia lakini sasa ni kiungo bora mkabaji, Fabinho alikuwa chachu kwa Monaco kutwaa taji Ligue 1, kadhalika kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mrefu, anayenyumbulika na mchezaji mahiri, Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa kwenye rada za Manchester United lakini sasa kuna mazungumzo kuwa Januari PSG na Juventus zinataka kumsajili mchezaji huyo anayeingia kwenye orodha ya Goal 50 kwa mara ya kwanza.

40. Gonzalo Higuain

Kulikuwa na vita kubwa na ghadhabu pale Juventus walipotoa kitita cha rekodi cha €90 milioni kumsajili Gonzalo Higuain kutoka kwa mahasimu wao Napoli, lakini Mwargentina huyo ametumia muda mchache kuanza kulipa bei hiyo aliyonunuliwa.

Amewapatia Juventus magoli 32 katika michuano yote waliposhinda mataji mawili, akifunga mara tano kwenye Ligi ya Mabingwa Waitaliano hao walipoangukia pua fainali. Hii ni pamoja na magoli mawili muhimu katika ushindi wa 2-0 mechi ya kwanza nusu fainali dhidi ya Monaco.

39. Alex Sandro

Alex Sandro anatokea kwa mara ya kwanza Goal 50 kufuatia msimu ambao ameendelea hadi kuwa beki bora wa pili wa kushoto duniani baada ya Marcelo wa Real Madrid.

Kupandisha mashambulizi kwake kuliisaidia Juventus kucheza kwa mafanikio walipokosa-kosa kutwaa mataji matatu katika historia, na kutokana na ubora wake huo, Juventus walikataa ofa ya €70m kutoka Chelsea.

38. Marco Asensio

Hii ndiyo sababu wazo la kutaka kumwondoa Gareth Bale si tatizo kwa mashabiki wa Real Madrid na sababu ni Marco Asensio, ambaye anatokea kwa mara ya kwanza kwenye Goal 50.

Kinda huyo wa miaka 21 amekuwa miongoni mwa wachezaji wanaosisimua sana kuwahi kutokea Hispania miaka hii na baada ya kuchangia upatikanaji wa magoli 10 kwa Blancos msimu uliopita, ameingia kwenye kampeni za msimu huu pia kwa namna ya ajabu akisaidia kushinda Supercopa dhidi ya Barcelona.

37. Dele Alli

Dele Alli alikuwa na uhakika wa kutetea tuzo ya mchezaji kinda ya mwaka ya PFA, baada ya kurudia maajabu yake ya 2015-16 katika kampeni ambazo alicheza kwa kiwango kikubwa na kufunga mara 18 Ligi Kuu Uingereza.

Ni ajabu kuwa hakuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya wakubwa, kutokana na mchango wake mkubwa kwenye mashambulizi Tottenham wakimaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Uingereza msimu uliopita.

36. Manuel Neuer

Manuel Neuer amekuwa katika wakati mgumu mwaka uliopita, baada ya kupata majeraha mfululizo, lakini alipokuwa fiti, alithibitisha kuwa ni kipa mahiri – fagio katika mchezo wa zama hizi.

Mjerumani huyo alikuwa katika kiwango cha juu kwa Bayern Munich, ambako aliisaidia kutwaa Bundesliga tena, na hivyo kuingia kwenye Goal 50 kwa mwaka wa tano mfululizo – mafanikio makubwa kwa kipa huyo katika zama za soka la kisasa.

35. Christian Eriksen

Mmoja wa wachezaji wasiopewa heshima wanayostahili katika soka la kipindi hiki, Christian Eriksen ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya Goal 50.

Amekuwa muhimu kwa Tottenham kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu – akitoa pasi 15 na kufunga magoli nane – Mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark ameisaidia nchi yake kupata fursa ya kucheza mechi za mtoano kufuzu Kombe la Dunia baada ya kufunga mara sita mfululizo katika hatua ya makundi.

34. Romelu Lukaku

Romelu Lukaku mara zote ameonyesha kuwa ni mchezaji mwenye ubora wa kucheza soka la watu mahiri na amethibitisha hilo 2017.

Baada ya kumaliza msimu wake wa mwisho Everton kwa magoli 25, Mbelgiji huyo amepoteza muda mchache tu kuthibitisha ada yake ya uhamisho ya £75 milioni kutua Manchester United kwa kufunga magoli saba katika mechi zake saba za mwanzo Ligi Kuu Uingereza kwa miamba hao wa Ligi Kuu.

33. Dani Carvajal

Dani Carvajal kwa namna zote ni jina kubwa Real Madrid lakini umuhimu wake kwenye kikosi cha Mabingwa hao wa Ulaya umethibitika.

Pamoja na umahiri wake katika ukabaji, Muhispania huyo ametoa pasi 12 za goli katika michuano yote msimu uliopita, ikiwa ni pamoja na mechi tisa Ligi ya Mabingwa na si jambo la kushangaza kuwa Blancos wamempa mkataba mwingine hadi 2022 mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25.

32. Sadio Mane

Mashabiki wengi wa Liverpool walitilia mashaka hekima ya klabu yao kuilipa Southampton €41m kwa ajili ya Sadio Mane majira ya joto 2016, lakini hofu yao iligeuka kuwa imani, kwani Msenegali huyo alikuwa mchezaji muhimu wa Jurgen Klopp kwa haraka sana.

Winga huyo mwenye kasi amefunga mara 13 katika msimu wake wa kwanza Anfield, ikiwa ni pamoja na goli la ushindi katika Merseyside derby, kuisaidia Reds kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa na kumwezesha kutokea kwa mara ya pili mfululizo kwenye Goal 50.

31. Paul Pogba

Haikuwa rahisi kwa Paul Pogba kuthibitisha thamani yake ya €105m, lakini kiungo huyo wa Manchester United amefurahia kurejea Old Trafford akitokea Juventus.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa amefunga mara tisa na kutoa pasi sita za magoli katika michuano yote msimu uliopita, akiisaidia United kushinda Kombe la Ligi na Ligi ya Europa, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alifunga katika fainali dhidi ya Ajax iliyochezwa Solna.

30. Radamel Falcao

Radamel Falcao ambaye amekuwa na kiwango kikubwa sana aliishia kucheza kwa mkopo Manchester United na Chelsea, lakini amerejea kwenye makali yake akiwa Monaco mwaka jana.

Mkolombia huyo amefunga magoli 21 katika mechi 29 kuisaidia timu yake kushinda taji la Ligue 1, anaingia kwa mara ya nne kwenye orodha ya Goal 50 – Mara ya kwanza tangu 2013.

29. Bernardo Silva

Bernardo Silva ni fundi asiyetumia maguvu na miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Monaco kutwaa taji Ligue 1 akiwa ametoa pasi tisa za goli (bila kutaja magoli nane aliyofunga).

Umahiri wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 umevutia klabu nyingi za soka na si jambo la kushangaza kuwa Pep Guardiola aliishawishi Manchester City kutumia €50m kumsajli Mreno huyo majira ya joto.

28. David Luiz

Uamuzi wa Chelsea kumsajili tena David Luiz kwa £34 milioni mwaka jana kulishangaza mashabiki wa Uingereza, ambao walikuwa wakiamini kuwa beki huyo wa kati ni tatizo katika safu ya ulinzi.

Lakini bosi wa Blues, Antonio Conte alikuwa akijua fika namna gani atamtumia Mbrazili huyo na ameonyesha umuhimu wake klabu hiyo ilipotwaa taji la Ligi Kuu Uingereza.

27. Alexis Sanchez

Ni rahisi kuelewa ni kwa nini Arsenal walipambana kwa nguvu zote kuizuia Manchester City kumsajili Alexis Sanchez ambaye amekuwa hatari kwenye safu ya mashambulizi kwa Gunners msimu wote uliopita.

Licha ya kucheza kwenye timu ambayo iliweza kumaliza nafasi ya tano Ligi Kuu Uingereza, mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile amekuwa katika kiwango cha hali ya juu na kutajwa miongoni mwa washindani wa tuzo ya mchezaji wa mwaka wa PFA, shukrani kwa magoli yake 24 na pasi 11 kabla ya kuwa nyota wa mchezo katika mechi ya fainali Kombe la FA dhidi ya Chelsea.

26. Casemiro

Luka Modric na Toni Kroos wanaweza kujizolea sifa zote katika safu ya kiungo Real Madrid lakini Casemiro amekuwa mchezaji ambaye anaipa timu hiyo nguvu ya kutawala mchezo.

Mbrazili huyo amekuwa na tabia ya kufunga magoli muhimu msimu uliopita, ikiwa ni pamoja na goli lililowarejesha vijana wa Zinedine Zidane mstarini kushinda Ligi ya Mabingwa dhidi ya Juventus.

25. Dries Mertens

Bosi wa Napoli Maurizio Sarri alisema kuwa jambo moja tu lisilopendeza kuhusu Dries Merten kuwa nambari 9 ni kwamba hakuna aliyebaini haraka kuwa winga huyo wa Kibelgiji amekuwa mshambuliaji hatari wa kati.

Mertens amekuwa mahiri tangu alipoanza kuchezeshwa kati Oktoba mwaka jana kutokana na majeraha ya Arkadiusz Milik, na kufunga mara 26 katika mechi 29 Serie A na alifanikiwa kumaliza kwa jumla ya magoli 28 katika mechi 35 hadi mwisho wa msimu.

24. Ousmane Dembele

Uibukaji wa Ousmane Dembele tunaweza kusema amepanda kwa kasi kama kimondo, baada ya kufanikiwa kuhamia Barcelona kwa kitita cha €105m (na nyongeza ya €40m) ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kujiunga na Borussia Dortmund kwa €15m.

Ada yake imekuwa kichekesho lakini winga huyo mwenye umri wa miaka 20 bila ubishi amekuwa na mwanzo wenye kusisimua msimu wake wa kwanza Signal Iduna Park, akifunga magoli sta na kutoa pasi 13 na kutwaa tuzo ya Bundesliga ya Rookie ya mwaka, na kuwa nyota wa mchezo BVB wakitwaa DFB-Pokal fainali dhidi ya Eintracht Frankfurt.

23. Antoine Griezmann

Ni mara ya tatu mfululizo kwenye Goal 50 kwa Antoine Griezmann, ambaye anaendelea kuufanya mwepesi mzigo mzito kwa kuipa makali safu ya mashambulizi ya Atletico Madrid kwa nguvu zake binafsi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, shabaha ya Manchester United, ambaye alifikia maamuzi ya kubaki Vicente Calderon baada ya Atleti kufungiwa usajili, amefunga magoli 26 katika michuano yote msimu uliopita, na pia amefunga mara nne kuiwezesha Ufaransa kufuzu fainali za Kombe la Dunia Urusi.

22. Edinson Cavani

Edinson Cavani amefurahia maisha yake ya soka baada ya kupewa majukumu ya kucheza kama mshambuliaji wa kati Paris Saint-Germain kufuatia Zlatan Ibrahimovic kuondoka kujiunga na Manchester United.

Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Uruguay alilazimika kucheza pembeni kutokana na uwepo wa straika huyo wa Sweden, na alifanikiwa kufunga magoli 49 katika mechi 50 kwenye michuano yote msimu uliopita, ikiwa ni pamoja na nane katika Ligi ya Mabingwa, na pia ameisaidia nchi yake kufuzu Kombe la Dunia 2018.

21. Zlatan Ibrahimovic

Zlatan Ibrahimovic ameendelea kuonyesha kuwa umri ni namba tu, straika huyo ameingia kwa mara ya tisa Goal 50 – Cristiano Ronaldo na Lionel Messi pekee ndio walitokea mara nyingi zaidi – shukrani kwa msimu bora wa kwanza akiwa Manchester United.

Kwa kweli, pamoja na kuwa kampeni zake ziliisha vibaya kwa majeraha, mkongwe huyo wa miaka 36 amefanya mengi - magoli 28, ikiwa ni pamoja na goli la ushindi katika fainali ya Kombe la Ligi – vilitosha kumshawishi Jose Mourinho kumpa mwaka wa pili Old Trafford ilipofahamika kuwa Ibrahimovic atapona haraka majeraha yake ya kano ya goti.

20. Luis Suarez

Luis Suarez inawezekana hakufanikiwa kucheza katika kiwango chake 2016, alipomaliza nafasi ya pili akitokea mara ya sita kwenye matoleo saba yaliyopita ya Goal 50, lakini nyota huyo wa Barcelona na Uruguay bado alifanikiwa kuzifungia mabao klabu na nchi yake msimu uliopita.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alifunga magoli 37 katika michuano yote kwa Blaugrana pekee, na kuifungia mara mbili Celeste katika harakati za kufuzu Kombe la Dunia 2018 wakishinda 4-2 dhidi ya Bolivia.

19. Robert Lewandowski

Bayern Munich huenda kwa ujumla wao walicheza chini ya kiwango mwaka uliopita lakini Robert Lewandowski hakuathirika na hilo, Mpolandi huyo ameingia Goal 50 kwa mara ya sita kutokana na kiwango chake safi.

Straika huyo amefunga mara 30 katika mechi 33 kwenye kampeni ambazo Wabavaria hao walitwaa taji la Bundesliga kabla ya Cristiano Ronaldo kumpiku katika mbio ya mfungaji bora Ulaya kufuzu Kombe la Dunia 2018, kwa magoli 16.

18. Pierre-Emerick Aubameyang

Moja ya mambo ya ajabu kufanyika kwenye soko la uhamisho wa majira ya joto ambako mamilioni yalitolewa kwa wachezaji wa kawaida ni kwamba hakuna hata klabu moja kubwa ya Ulaya iliyojaribu kumsajili Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye anatokea mara ya pili mfululizo kwenye 20 bora ya Goal 50.

Straika huyo wa Borussia Dortmund alimzidi Robert Lewandowksi na kumaliza kinara wa mabao kwenye chati ya Bundesliga, akiwa na magoli 31 katika mechi 32 tu, kabla ya kushinda DFB-Pokal dhidi ya Eintracht Frankfurt.

17. Harry Kane

Kipanga wa Tottenham Hotspur Harry Kane amethibitisha kuwa ni miongoni mwa washambulizi mahiri kwenye ulimwengu wa soka baada ya kufunga zaidi ya magoli 20 kwenye Ligi Kuu Uingereza mwaka wa tatu mfululizo.

Msimu uliopita ulikuwa mzuri sana kwake, Muingereza huyo alifunga mara 29 katika mechi 30 tu, na Kane ameendeleza kiwango chake safi msimu huu, sasa kuna tetesi kuwa Madrid wapo mbioni kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24.

16. Thiago Alcantara

Carlo Ancelotti amefanya makosa chungu nzima alipokuwa kocha wa Bayern Munich lakini uamuzi wake kumpeleka Thiago Alcantara mbele umesaidia sana.

Kiungo huyo mkabaji ambaye amekumbwa na majeraha mara kwa mara alifurahia msimu ambao huenda ni bora katika maisha yake ya soka, amepiga pasi nyingi zaidi katika nusu ya wapinzani kuliko mchezaji yeyote Bundesliga msimu uliopita (1,393) na hiyo ni asilimia 87.3.

15. Leonardo Bonucci

Leonardo Bonucci huenda hajawa na mwanzo mzuri sana AC Milan lakini beki huyo alikuwa katika kiwango safi kampeni za 2016-17 akiwa Juventus.

Pamoja na kuwa kiungo cha kati, Muitaliano huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi zenye macho amefunga magoli matano, ikiwa ni pamoja na goli muhimu la pili katika ushindi wa Coppa Italia fainali dhidi ya Lazio, na pia alikuwa kizingiti dhidi ya Barcelona kufuzu fainali Ligi ya Mabingwa.

14. Dani Alves

Bila shaka Barcelona walifanya kosa kubwa sana kwenye uhamisho katika historia yao kumruhusu Dani Alvesi ambaye anatokea kwa mara ya sita Goal 50 – kuondoka bure majira ya joto mwaka jana kujiunga na Juventus.

Beki huyo wa kulia wa Kibrazili alikuwa kiini cha Bianconeri kutwaa mataji mawili, akifunga goli la kwanza fainali Coppa Italia, lakini pia aliiwezesha timu yake kushinda nusu fainali Ligi ya Mabingwa dhidi ya Monaco kwa goli moja na pasi tatu za mwisho.

13. Isco

Mwerevu na mwenye weledi, fundi, Isco alikuwa mahiri sana kwa Real Madrid nusu ya pili msimu uliopita kiasi ambacho hata Gareth Bale alipokuwa fiti kamili kwa fainali ya Ligi ya Mabingwa, nyota huyo wa Wales hakupata nafasi kikosi cha kwanza.

Alipata fursa ya kucheza mara kwa mara kutokana na matatizo ya muda mrefu ya majeraha kwa winga huyo, Isco alifanikiwa, akifunga magoli muhimu kwenye mbio za ubingwa wa La Liga, goli la kukumbukwa zaidi likiwa dhidi ya Sporting Gijon na Ligi ya Mabingwa nusu fainali dhidi ya Atletico.

12. Eden Hazard

Baada ya kufanyiwa uamsho na bosi mlezi wa Chelsea Guus Hiddink mwishoni mwa kampeni za 2016-16, Eden Hazard alirejea katika ubora wake chini ya bosi mpya Antonio Conte msimu uliopita, na kuiwezesha Blues kutwaa taji Ligi ya Uingereza.

Winga huyo mahiri wa Ubelgiji alifurahia msimu wa Ligi Kuu Uingereza, akifunga mara 16 na kutengeneza magoli matano, na kufanikiwa kuingia Goal 50 kwa mara ya tano.

11. Marcelo

Ikiwa kuna beki muhimu zaidi katika soka la zama za kileo, ni Marcelo, ambaye amekuwa kiungo muhimu kwa Real Madrid katika ligi na Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Mbrazili huyo alitengeneza magoli 10 katika La Liga pekee, ikiwa ni pamoja na manne kwa ajili ya Cristiano Ronaldo, hiyo ni ishara ya maelewano mazuri baina yao dimbani, lakini pia alifunga goli muhimu dhidi ya Valencia katika mbio za ubingwa.

10. Toni Kroos

Akiwa na umri wa miaka 27 tu, Toni Kroos ameendelea kuonyesha kuwa ni miongoni mwa wachezaji bora katika historia ya soka, kiungo huyo mwenye vionjo adimu alipokuwa chini ya Pep Guardiola Bayern Munich alisajiliwa Real Madrid kwa gharama ya €25m tu.

Msimu uliopita, mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2014 alikuwa Mjerumani wa kwanza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara tatu, baada ya kushirikiana vema na Luka Modric na Casemiro kuamua ubingwa dhidi ya Juventus.

Kroos alikuwa na ushawishi mkubwa katika mafanikio ya Madrid kwenye La Liga, akitoa pasi 12 za goli, pia akifunga magoli muhimu katika kazi yake mwishoni mwa msimu dhidi ya Sevilla na Celta Vigo.

9. Paulo Dybala

Akielezewa kama mrithi wa Lionel Messi kwa Argentina, Paulo Dybala ameibuka na kung’ara alipomfunika Mwargentina mwenzake Juventus ikiisambaratisha Barcelona kwa kipigo cha 3-0 katika mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa.

Dybala alifunga magoli mawili na kuifanya beki ya Barca ionekane haifanyi kitu, kwa ustadi na fimbo ya miujiza ya mguu wake wa kushoto Juve wakiwaweka kwenye upanga wapinzani wao mjini Turin.

Mchezaji huyo mwenye dalili njema kushinda Goal 50 siku za mbeleni, ‘La Joya’ alikuwa na ushirikiano mzuri na Gonzalo Higuain, Bianconeri walishinda Scudetto na Coppa Italia na kwa msaada wake walikosa-kosa kunyakua mataji matatu baada ya kufungwa na Real Madrid fainali Ligi ya Mabingwa.

8. N'Golo Kante

Hakuna kauli kubwa kuhusu kipaji na ushawishi wa N’Golo Kante zaidi ya ukweli kwamba amedumu Uingereza kwa miaka miwili na kila msimu ameumaliza na medali shingoni mwake.

Naam, Chelsea hawawezi kuamini kuwa walipata bahati kwamba Leicester walihitaji £32m tu kwa ajili ya msingi ambao juu yake mafanikio ya ubingwa wa kihistoria yalijengwa na Kante kwa haraka sana alionyesha kuwa na nguvu ya uharibifu dhidi ya timu pinzani na kuwapa nafasi Eden Hazard na wenzake kuonesha umahiri wao bila hofu kuhusu kazi ya safu ya ulinzi.

Umahiri wake ulimpatia tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa PFA, FWA na Ligi Kuu.

7. Kylian Mbappe

Imedhihirika tangu Kylian Mbappe alipomrithi Thierry Henry kama mchezaji kinda zaidi kuwahi kucheza Monaco (Disemba 2015) na mfungaji kinda zaidi (Februari 2016) ni kipaji mahususi.

Kwa umahiri wake tu, ingawa amethibiti mwaka huu, kama mchezaji asiye na woga, mwenye kasi, aliiwezesha Monaco kutwaa taji la kwanza Ligue 1 baada ya miaka 17, kwa magoli 15 na pasi 11 za goli, pamoja na magoli sita katika mechi sita za kwanza hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa.

Louis Saha anasema straika huyo mpya wa Paris Saint-Germain ni bora zaidi ya Henry katika umri wake wa miaka 18, wakati Ludovic anasisitiza kuwa amepevuka kuliko Messi katika umri sawa. Lakini labda Andrea Barzagli ameiweka vizuri zaidi aliposema ulinganishi huo hauna mashiko, akisema, “Sijawahi kuona mtu kama Mbappe kabla!”

6. Neymar

Kwa mara ya pili mtawalia anashika nafasi ya sita Goal 50 na mara ya saba mfululizo kwa Neymar katika orodha hii, ambaye mwaka huu amekuwa mchezaji ghali zaidi duniani Paris Saint-Germain walipotoa €222m kuununua mkataba wake Barcelona.

Ada hiyo inaweza kuwa kichekesho, lakini ni rahisi kuelewa ni kwa nini klabu hiyo inayomilikiwa na Qatari ilikuwa tayari kumsajili Mbrazili huyo, kufuatia kile alichofanya kuirejesha Barca kwenye mstari michuano ya Ligi ya Mabingwa katika historia msimu uliopita hatua ya 16-Bora wakishinda dhidi ya PSG.

Zaidi ya hayo, baada ya kuunda utatu hatari katika mashambulizi ambao haujawahi kutokea Camp Nou, sasa anataka kufanya hivyo PSG, baada ya kuanzisha ushirikiano mzuri na Kylian Mbappe na Edinson Cavani katika Parc des Princes.

5. Sergio Ramos

Mabeki wachache katika historia wamekuwa na ushawishi katika Nyanja zote dimbani kama Sergio Aguero, ambaye alimaliza msimu kwa kufunga magoli 10 kwenye michuano yote kwa kuwa mchezaji wa kwanza kuiongoza Real Madrid kutwaa La Liga na Kombe la Ulaya tangu Juan Alonso mnamo 1958.

Pamoja na kuipatia sare muhimu ya Clasico Real Madrid katika Barcelona baada ya mwendo wa mechi 40 bila kufungwa, Muhispania huyo pia alifunga magoli muhimu dhidi ya Real Betis kwenye La Liga na Napoli Ligi ya Mabingwa.

Akiwa na umri wa miaka 31, Ramos anacheza katika kiwango cha juu kila siku, nafasi ya tano ni ya juu zaidi kwake kuwahi kumaliza katika Goal 50, akiwa anaingia kwa mara ya saba kama beki mahiri.

4. Lionel Messi

Lionel Messi anakosa tatu bora katika Goal 50 lakini huu ulikuwa mwaka wenye mvuto kwa Nambari 10 huyu, angalau kwa mtazamo binafsi.

Hakuna mtu aliyefunga magoli mengi 2017 zaidi ya mshambuliaji huyo wa Barcelona na Argentina, ambaye pia amekuwa na kiwango cha kipekee baada ya kuiongoza klabu yake kushinda dhidi ya Real Madrid kwa magoli mawili kunako dimba la Santiago Bernabeu, na kwa jitihada zake binafsi ameiwezesha nchi yake kufuzu Kombe la Dunia 2018 kwa hat-trick dhidi ya Ecuador mjini Quinto.

Msimu mgumu katika Camp Nou uliwapa taji moja tu, Copa del Rey, lakini Messi alimaliza pia kama mfungaji bora wa michuano hiyo (5) na La Liga (37 katika mechi 34 tu!) na kuondoka na kiatu cha dhahabu.

3. Luka Modric

Andriy Shevchenko hivi karibuni alimwelezea Luka Modric kama “mmoja wa viungo mahiri zaidi kuwahi kutokea” na ni vigumu kuikataa kauli ya legendari huyo wa AC Milan.

Akisajiliwa na Real Madrid 2012 kwa kiasi ambacho kwa sasa kinaonekana kuwa fedha kichele €30m, Mcroatia huyo amekuwa mchezaji bora mno katika zama za soka la kisasa, mchezaji muhimu sana kwa Blancos ambao wanaonekana kuwa timu tofauti bila ya mkongwe huyo wa miaka 32 kikosi cha kwanza.

Modric alikuwa na ushawishi mkubwa katika fainali ya Ligi ya Mabingwa, mechi ambayo alikuwa na umiliki mkubwa muda baada ya muda, wakigeuza matokeo ya 1-1 hadi mapumziko kuwa 4-1 hadi filimbi ya mwisho.

Nafasi katika jukwaa la Goal 50, ni thawabu tu kwa mchezaji huyo anayeonekana kuwa mahiri katika nyanja mbalimbali ikilinganishwa takribani na kila mmoja dimbani.

2. Gianluigi Buffon

Gianluigi Buffon amemaliza katika nafasi ya juu zaidi katika historia ya Goal 50 kufuatia msimu bomba kwa klabu yake alipoitumikia kama legendari 2016-17.

Nahodha huyo wa Bianconeri alikuwa mchezaji thabiti timu yao iliposhinda mataji mawili ya nyumbani na Scudetto kwa mara ya sita mfululizo.

Licha ya kutimiza miaka 39 Januari, mchezaji huyo anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi Italia aliiongoza Juve fainali ya pili Ligi ya Mabingwa ndani ya miaka mitatu.

Aliruhusu magoli matatu tu hadi Juve ilipofika fainali Cardiff na alicheza mechi 600 bila kuruhusu goli katika michuano hiyo, tukio la kukumbukwa zaidi katika kipindi chake cha soka ni kuokoa penalti ya Alexandre Lacazette katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Lyon.

Cha kusikitisha, Buffon ameshindwa kulitia mkononi taji la heshima katika maisha yake ya soka Juventus walipopoteza dhidi ya Real Madrid fainali – lakini anajifariji kwa kupata nafasi ya pili kwenye Goal 50.

1. Cristiano Ronaldo

Mashine halisi ya kufunga magoli, Cristiano Ronaldo amejipatia nafasi ya kwanza Goal 50 wa mwaka wa pili mfululizo, Supastaa huyo wa Kireno akiweka rekodi ya kushinda mara tano tuzo hii.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 amefunga mara 25 katika mechi 29 za La Liga ambako waliibuka washindi – ubingwa wao wa kwanza tangu 2012 – lakini, ulikuwa msimu wa mafanikio makubwa kwa klabu ambako alithibitisha umahiri wake.

Winga huyo wa zamani wa Manchester United alifunga hat-trick mfululizo katika mechi za mtoano Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich na Atletico Madrid, kabla ya kuishindia taji Madrid kwa mabao mawili fainali dhidi ya Juventus.

Hii inamaanisha kuwa mwakani Real watakuwa wakitafuta ushindi wa tatu mfululizo wa Kombe hilo la Ulaya wakati Ronaldo akiwa anatafuta tuzo ya tatu mtawalia Goal 50 – Je! Itakuwa hivyo?